karibu Makazi solution kwa mahitaji ya viwanja.

karibu Makazi solution kwa mahitaji ya viwanja.

Breaking News

Asili ya kabila la warangi wilayani Kondoa

Warangi ni moja ya makabila ya Kibantu. Pia huwekwa kwenye kundi la Wabantu lijulikanalo kama kundi la Niger-Congo. Kabila la Warangi lilianza lini, bado ni suala la mdahalo kwani wanasayansi wa isimu na historia bado hawajafikia mwafaka. Wengine husema kwamba kabila la Warangi lilianza kati ya miaka 300 baada ya Kristo. Na nadharia hii inashikiliwa sana na Ehitna. Na kwa upande mwingine Kesby husema kwamba kabila la Warangi lilianza kati ya miaka 1500 na 1700. Nadharia hii hushauri kwamba kabila la Warangi lilianza miaka 300 tu iliyopita. Kati ya nadharia zote hakuna nadharia hasa ambayo ipo sahihi ila zote zinajaribu kutusaidia kupata ukweli wa hali halisi tu wa kabila la Warangi. Hata hivyo lengo langu katika matini hii si kujaribu kujiingiza katika historia ya kabila la Warangi bali ni kutaka kukupa historia fupi ya Warangi.

Kabila la Warangi hupatikana katika wilaya ya Kondoa iliyopo mkoani Dodoma. Katika wilaya ya Kondoa Warangi hasa hupatikana kuanzia sehemu za Kidoka km 60 kutoka Kondoa mjini hadi Bereko km 60 kwa upande wa kaskazini.
Katikati ya eneo hili ndiyo hasa eneo ambapo Warangi hupatikana. Kwa upande wa mashariki eneo Warangi hupatika katika vijiji vingi mpaka sehemu za Mrijo Chini km 70 kutoka Kondoa mjini. Kuna vijiji vingi ambapo Warangi hupatikana vikiwemo vijiji vilivyopo kwenye barabara ya duara ichepukayo kwa upande wa mashariki sehemu za Bicha na kuunganika kwa upande wa kaskazini katika eneo la Kolo, sehemu yenye michoro ya kale ya mapangoni.

Tukirudi katika historia, Warangi wana historia tatu zinazohitilafiana kuhusu uasili wao hasa. Nadharia za historia hizo ni;


HISTORIA YA KWANZA.
Warangi walisafiri kutoka upande wa magharibi na mpaka kufika sehemu za Galapo. Baada ya kuweka makao sehemu hizo, waliendelea kutafuta eneo zuri la kuishi. Katika wakati huo vijana wa Kirangi walikuwa hutembea kwa ajili ya kutafuta sehemu hasa ambayo wangeweza kufanya makazi ya kudumu. Kuhama hama kwa Warangi kulisababishwa hasa na mambo mawili ambayo ni;

(a)Vifo vya watoto.
Warangi walipohamia mahali fulani na kugundua kwamba watoto walikuwa wakifa wakiwa bado wadogo au wachanga walihama. Hii ni kwa sababu sehemu ambapo watoto wachanga walikuwa hawaponi hapakufaa kwani palihatarisha uwepo wa kabila kwa siku za baadae. Kutokana na masimulizi inawezekana vifo vya watoto vilisababishwa na ugonjwa wa malaria ambao husababisha sana vifo vya watoto hata leo.

(b)Mavuno mazuri ya chakula.
Sehemu ambayo ilikuwa kame sana kwa Warangi haikufaa, kwani kwa asili wao walitegemea kilimo kwa ajili ya ustawi wao. Kwa hiyo sehemu ambayo haikuwa na chakula cha kutosha haikuwafaa. Hivyo walisonga mbele kutafuta sehemu nzuri zaidi.


Kwa hiyo kutoka na kusafiri kwa vijana hao, walifika katika milima ambayo hata sasa hujulikana kama milima ya Mʉlaanga. Baada ya kusafiri walifika katika kijiji kijulikanacho kwa sasa kama Sambwa. Jina hili lilitokana na wazee waliosema kwamba kuhama watu wote kuelekea katika kijiji hicho halikuwa wazo zuri kwani inawezekana kukawa na ugonjwa wa kufisha katika sehemu hiyo. Hivyo wazee walishauri wahame watu wachache ili kuangalia kama nchii hiyo ni haribifu yaani saambʉ kwa Kirangi.
Walikaa na muda ukaenda bila kupata madhara yoyote wao pamoja na mifugo yao. Hivyo wakasema sasa tuhame kwenda kwenye nchi ile tuliyodhani ni ya uharibifu kwa hiyo wakaendelea kuiita Saambwa.

Kutokana na kuzaliana na kukua kwa kabila ardhi ilianza kutotosheleza na hivyo waliendelea sasa kutafuta makazi zaidi.
Na kama kawaida vijana walisafiri na kupanda milima na hapo ndipo walipofika katika eneo ambalo kwa sasa huitwa Haubi.
Walipofika katika eneo hili walikuta kuna maji yaani ihau na nchi ilikuwa tulivu tena ilifaa sana kwa watoto kwani sasa hapakuwa kabisa na tatizo la watoto kufa. Sababu hasa ya watoto kutokufa yawezekana ikawa ni kutokana na baridi kali ambayo ilifanya sehemu hii isiwe na malaria kabisa. Kwa sababu hiyo basi Warangi walifanya makazi ya kudumu hapa.

HISTORIA YA PILI.
Warangi hutoa historia ya kwamba walitoka sehemu za kaskazini. Yaani sehemu za Ethiopia na kufuata bonde la ufa hadi kufika eneo la mlima Kilimanjaro. Katika mlima Kilimanjaro, Warangi hawakuishi kwa muda mrefu kutokana na kuwa kwamba zao lao kuu la uwele lilisitawi vizuri lakini masuke hayakuwa na punje.
Hii labda ilisababishwa baridi na na utomvu utokanao na fangasi. Ugonjwa huu hufanya masuke kutoa aina fulani ya punje nyeusi ambazo ukishika hutoa kitu kama moshi. Kwa sababu hiyo Warangi waliamua kuhama na kuendelea na safari yao. Katika safari yao walisafiri hadi kufika milima ya Usambara.
Lakini kutokana na zao lao la chakula kutositawi vizuri katika maeneo ya milima ya Usambaa.

Watu hawa waliendelea kuhama na ndipo waliposafiri hadi kufika sehemu za Manyara na hatimaye Babati sehemu za Galapo. Kutoka hapo masimulizi huendelea kama ilivyo katika historia ya kutoka magharibi iliyoelezwa hapo juu.

HISTORIA YA TATU.




Kuna dhana kwamba Warangi walisafiri kutoka sehemu za kusini. Na hii hasa huletwa na dhana kwamba Warangi walitokana na kumeguka kwa makabila ya kusini na walisafiri kutoka huko na kufanya makazi yao katika sehemu za Gairo mkoani Morogoro.
Dhana hii hupewa uzito hasa kutokana na mlima uliopo sehemu za Gairo uitwao mlima wa Warangi hata leo. Katika safari hiyo husemekana kwamba Warangi walisafiri kutoka sehemu hizo kwa kufuata milima ya Kibakwe na kwenda kaskazini, kupitia sehemu za Mtungutu, Chemba, Kelema na hadi kufika sehemu za Busi na Sambwa. Baada ya kufika Sambwa masimulizi sawa na nadhari ya kwanza iliyoelezwa hufanana.

Kutokana na nadharia zote tatu, nadharia ya kwamba Warangi walitoka kusini yawezekana isiwe halisia sana, kwani lugha ya Kirangi yafanana sana na lugha za Kisukuma ambapo asilimia 48% ya msamiati yafanana, Wanyamwezi asilimia 47% ya msamiati yafanana, Wanyiramba asilimia 54% ya msamiati yafanana na Wambungwe ambapo asilimia 74% ya msamiati yafanana. Ukilinganisha na makabila ya kusini yaani Wahehe ambapo ni asilimia 23% na Wabena 21%. Nadharia hii inatufundisha kwamba lugha tunazofanana sana kimsamiati na lugha ambazo tumeziacha siku za karibuni sana. Hivyo, Warangi inaonekana walitoka sehemu za magharibi.

Pia nadharia ya kutoka kaskazini yaweza kuwa inatokana na Warangi kuoana na makabila ya Wakushi yaani Waburunge, Wairaq na Waalagwa. Hivyo katika historia na masimulizi ya watoto waliozaliwa katika familia ambapo wazazi walitoka katika sehemu mbalimbali masimulizi ya kutoka magharibi yalianza kuzorota na watoto kupata masimulizi ya kutoka kaskazini.
Pia ukizingatia mara nyingi katika kuoana wanawake wa Kikushi waliolewa sana na Warangi. Kutokana na sababu ya kwamba watoto walikuwa hukaa muda mwingi na mama zao hivyo walipata masimulizi ya upande mmoja na kusababisha masimulizi ya upande wa magharibi yazorote kabisa.
Zaidi sana, dhana ya Warangi kutoka kaskazini huambatana na nadharia za kidini kwani baadhi ya Warangi husema wao huitana mwaana maka, wakikumbuka sehemu walizotoka, yaani sehemu za Makka.

Hata hivyo kutokana na kabila la Warangi kuwa kabila la Wabantu dhana ya kuwa walitoka sehemu ya kaskazini si kweli kwani asili hasa ya Wabantu ni Kongo. Hivyo dhana ya Warangi kutoka sehemu za magharibi huendena na dhana ya historia ya makabila yote ya Kibantu. Lakini pia kutokana na kuoana na makabila mengine bado Warangi wanaweza kujivunia historia ya kutoka kaskazini kwani hii pia ni moja ya asili yao.

No comments